
…Hatua ya serikali ya kufunga mawasiliano kwa sura moja inatafsiriwa na wachambuzi kama njia ya kuimarisha ujumbe wa serikali na kudhibiti upotoshaji.
Soma pia: Muyumba Aikosoa Mkataba wa Washington
Lakini pia imeibua maswali kuhusu uwazi wa mchakato wa amani huo.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC) imeamua kuweka udhibiti mkali kwenye mawasiliano yote yanayohusu mkataba wa amani uliotiwa saini na Rwanda tarehe 27 Juni mjini Washington, Marekani. Tangazo hili limetolewa rasmi usiku wa Jumapili, Julai 6, na Ofisi ya Waziri Mkuu Judith Suminwa Tuluka.
Kulingana na taarifa hiyo, ni taasisi tatu tu ndizo zenye mamlaka ya kuzungumza rasmi kuhusu mchakato wa upatanishi kati ya serikali ya Congo na kundi la waasi la M23, pamoja na kuhusu mkataba wa amani uliosainiwa kati ya Kinshasa na Kigali. Taasisi hizo ni:
- Wizara ya Mambo ya Nje inayoongozwa na Waziri Thérèse Kayikwamba Wagner
- Wizara ya Mawasiliano inayoongozwa na Waziri Patrick Muyaya
- Idara ya Mawasiliano ya Ikulu ya Rais
Primature imeeleza kuwa lengo la hatua hii ni “kudhibiti na kulinda mawasiliano ya serikali” hasa katika kipindi hiki kigumu cha mazungumzo ya kidiplomasia, ili kuepuka upotoshaji wa habari au taarifa zisizo rasmi.
Mkataba wa Washington, uliosainiwa mbele ya Marekani, umekuwa gumzo kubwa nchini Congo, huku wananchi, wachambuzi wa siasa, na viongozi wa upinzani wakiendelea kuuliza maswali kuhusu undani wake na jinsi utakavyotekelezwa.
Wengi wamepongeza hatua ya serikali ya kuhakikisha taarifa zinatolewa kwa sauti moja, lakini baadhi wanahoji kama hatua hiyo inaweza kupunguza uwazi kwa umma kuhusu makubaliano hayo nyeti.
Serikali ya Congo inaendelea kusisitiza kuwa lengo ni kuleta amani ya kudumu katika eneo la mashariki mwa nchi, lakini mchakato huo unaendelea kufuatiliwa kwa karibu na wananchi wa Congo na jamii ya kimataifa.
Chanzo: BBC – Congo-Rwanda Peace Agreement
