
Kasaï: Wagonjwa wa M-pox Wathibitishwa Gerezani Tshikapa
Wizara ya Afya ya mkoa wa Kasaï imethibitisha kuwa kuna visa vitano vya maambukizi ya virusi vya M-pox katika gereza kuu la Tshikapa, mji mkuu wa mkoa huo. Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Afya wa mkoa huo, Odette Nkama Mekanda, alipofanya ziara maalum kwenye gereza hilo.
Kwa mujibu wa mamlaka za afya, visa hivi viligunduliwa baada ya kutolewa kwa tahadhari ya uwepo wa dalili za ugonjwa huo miongoni mwa wafungwa. Kufuatia hali hiyo, waziri huyo alikabidhi msaada wa haraka wa madawa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa waliothibitishwa.
“Katika maagizo tuliyopewa na Gavana, tulikuja kutathmini hali halisi na kuchukua hatua za dharura ili kuzuia kusambaa zaidi kwa virusi hivi kwenye mazingira haya yaliyofungwa,” alisema Waziri Nkama.
Mbali na madawa, serikali ya mkoa iliahidi msaada wa ziada ukiwemo magodoro kwa ajili ya kulaza wagonjwa, pamoja na vifaa vingine vya afya muhimu kwa matibabu.
Msongamano mkubwa na ukosefu wa usafi wa mazingira katika magereza bado vinaendelea kuwa sababu zinazoongeza hatari ya milipuko ya magonjwa, hali inayoyafanya magereza kuwa maeneo yenye udhaifu mkubwa kiafya.
Mamlaka za afya zimehimiza umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa kiafya na kuboresha mazingira ya maisha ya wafungwa ili kudhibiti maambukizi zaidi. Hatua hizi ni sehemu ya mkakati wa dharura uliowekwa na mkoa wa Kasaï kwa ajili ya kukabiliana haraka na milipuko ya magonjwa yenye uwezo wa kusambaa kwa kasi kwenye maeneo yenye msongamano kama magereza.
Mwandishi: Mangwa
