
Ripoti ya UN: Jeshi la Uganda Latekeleza Operesheni Nje ya Makubaliano Mashariki mwa Congo
Katika hali inayozua taharuki, ripoti mpya ya kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa Julai 2025 imebaini kuwa Jeshi la Uganda (UPDF) limeongeza kwa kiasi kikubwa uwepo wake katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini, na maeneo ya mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), nje ya mipaka ya operesheni rasmi ya pamoja ya Shujaa dhidi ya waasi wa ADF.
Ripoti hiyo imefichua kuwa kati ya Februari na Machi 2025, Uganda ilituma zaidi ya wanajeshi 1,000 na vifaa vizito vya kijeshi katika maeneo ya Bunia, Mahagi, na Djugu bila idhini rasmi ya serikali ya Congo. Operesheni hiyo, iliyoongozwa na Jenerali Felix Busizoori, haikuwa sehemu ya mkataba wa Shujaa uliosainiwa kati ya FARDC na UPDF.
Malengo ya Biashara na Madini Nyuma ya Operesheni
UPDF ilidai kuwa inawalinda raia wa jamii ya Hema dhidi ya mashambulizi ya kundi la CODECO. Hata hivyo, ripoti hiyo imebaini kuwa malengo ya Uganda yalizidi mipaka ya ulinzi wa raia na yalihusiana zaidi na maslahi ya kibiashara kama biashara ya dhahabu, mafuta ya Ziwa Albert, na ushawishi wa kiuchumi katika eneo hilo.
Mvutano na Makundi ya Ndani
Uwepo wa majeshi ya Uganda ulichochea mapigano makali na kundi la waasi la CODECO/URDPC. Mnamo Machi, UPDF iliweka kambi katika maeneo ya Fataki kwenye barabara ya RN27, hatua ambayo ilisababisha mapigano ya wiki kadhaa na mashambulizi ya mabomu yaliyoharibu vijiji vya jamii ya Lendu.
Ripoti imeeleza kuwa matamshi ya kijeshi ya Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mkuu wa majeshi ya Uganda na mwana wa Rais Yoweri Museveni, yamezidisha hali ya mivutano kwa kuunga mkono jamii ya Hema na kutishia kundi la CODECO.
Changamoto kwa MONUSCO
Ripoti hiyo imeonya kuwa uwepo wa UPDF unakinzana na operesheni za MONUSCO katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani, na kuna ukosefu wa uratibu wa kijeshi kati ya vikosi hivyo viwili.
Makubaliano Mapya ya Shujaa
Kufuatia sintofahamu hiyo, tarehe 20 Juni 2025, Jenerali Muhoozi Kainerugaba na Jenerali Jules Banza wa FARDC walitia saini makubaliano mapya ya operesheni Shujaa, yanayoruhusu kupanua mashambulizi dhidi ya ADF hadi maeneo ya Mambasa, Djugu, Irumu, Mahagi, na Aru.
Makubaliano hayo yanasisitiza kuimarisha uratibu wa kiusalama na kulinda miradi muhimu ya miundombinu kama ujenzi wa barabara ya Kasindi-Beni-Butembo.
MANGWA

