
RDC: Francine Muyumba Aikosoa Vikali Mkataba wa Washington, Amtumia Mandela Kutoa Onyo
Francine Muyumba, aliyewahi kuwa seneta wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC), ametoa ukosoaji mkali kuhusu namna serikali ya Congo ilivyosimamia mkataba wa amani uliotiwa saini na Rwanda mnamo Juni 27, 2025, mjini Washington kwa usimamizi wa Marekani.
Kupitia chapisho kwenye mtandao wa X siku ya Ijumaa, Julai 4, Muyumba alidai kuwa:
“Serikali ya Congo imesaini mkataba ambao yenyewe haijui undani wake wala athari zake.”
Alieleza kuwa Kinshasa ilifanya uamuzi wa haraka bila kuchunguza kwa kina matokeo ya mkataba huo kwa taifa.
Akimlenga waziri wa Mawasiliano wa Congo, Patrick Muyaya, Muyumba alidai kuwa Muyaya, bila kujua, alisaidia taifa kuelewa mapungufu ya diplomasia ya Congo katika mchakato huu.
“Lengo lilikuwa kuonekana kando ya Rais wa Marekani, lakini utekelezaji wa mkataba huo umepuuzwa kabisa,” alisema akirejelea mkutano wa mwisho wa maelezo ya mkataba huo uliofanyika na Waziri Therese Wagner.
Muyumba alitumia maneno ya hekima ya Nelson Mandela kusema:
“Kusaini mkataba bila njia ya kuutekeleza ni sawa na kuahirisha mgogoro.”
Pia alieleza mashaka kuhusu nafasi ya Bunge la Congo katika mchakato huo: “Na Bunge la Congo lina nafasi gani katika haya yote?”
Kauli ya Muyumba imeibua mjadala mpana kuhusu uwazi, ushirikishwaji na uthabiti wa serikali katika maamuzi ya kimataifa yanayogusa mustakabali wa nchi.
Mwandishi: MANGWA
