DRC: Sakata la Harusi Yasitishwa Lubumbashi kwa Sababu ya Kukataa Kubusiana

Sakata lisilo la kawaida limeibuka mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya afisa wa ndoa kusitisha sherehe ya harusi kwa sababu ya kitendo kimoja kidogo lakini kilichoibua mjadala mkubwa – maharusi walikataa kubusiana hadharani kwa sababu ya imani yao ya kidini inayofuatilia mafundisho ya William Branham.

Tukio hili lililorekodiwa limeenea kwenye mitandao ya kijamii likisababisha maoni yanayogawanyika – baadhi wakiunga mkono hatua ya afisa huyo, wengine wakilaani vikali kile walichokiona kama unyanyasaji wa haki za kidini.

Wakati mjadala ukiendelea, wataalamu wa sheria wameeleza wazi kuwa busu si sharti la kisheria katika ndoa nchini Congo. Sheria ya familia ya Congo inaeleza kuwa ndoa ni mkataba wa kisheria unaohitaji ridhaa ya wahusika, ushuhuda wa mashahidi, na kutimiza masharti ya msingi kama vile umri na monogamia. Hakuna popote kwenye sheria inayotaja busu kuwa hitaji la kufanikisha ndoa.

Isaac Mukendi, naibu bwana meya wa Limete, alihoji kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter), “Busu lina uzito gani wa kisheria hadi ndoa isitishwe? Hii ni nguvu kupita mipaka ya afisa wa serikali.”

Kulingana na sheria za DRC, afisa wa ndoa hana mamlaka ya kufuta ndoa, isipokuwa tu kama kuna tatizo la msingi kama kutokuwepo kwa ridhaa au ndoa ya awali ambayo haijavunjwa. Uamuzi wa kusitisha au kufuta ndoa unaweza kutolewa tu na mahakama ya amani.

Tukio hili limefungua mjadala mkubwa juu ya haki za waumini wa madhehebu madogo, elimu ya maafisa wa serikali kuhusu sheria, na mpaka wa mamlaka ya utawala wa serikali. Ni tukio linaloonyesha changamoto kati ya mila zinazoendelea kuchipuka na imani za kidini zinazoshikilia misimamo ya kale.

Mwandishi: MANGWA