Daktari Obadi Musumba Afariki Baada ya Kupigwa Risasi Mjini Goma

Daktari Obadi Musumba, nguzo muhimu wa huduma za afya katika eneo la Karisimbi, amefariki dunia Jumamosi, tarehe 5 Julai 2025, katika hospitali ya CBCA Bethesda mjini Goma. Alifariki kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mnamo usiku wa tarehe 26 hadi 27 Mei mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa, Dkt. Musumba alipigwa risasi tatu – kwenye nyonga, mgongoni na miguuni – akiwa njiani kurejea nyumbani katika mtaa wa Virunga, wilaya ya Karisimbi. Baada ya kushambuliwa, alipelekwa hospitali ya CBCA Virunga kwa matibabu ya dharura, kabla ya kuhamishiwa CBCA Bethesda kwa uangalizi maalum. Licha ya juhudi kubwa za madaktari, hali yake iliendelea kuwa mbaya hadi alipofariki.

Tukio hili linaongeza msururu wa matukio ya uhalifu dhidi ya wahudumu wa afya katika mji wa Goma, huku wimbi la mashambulizi ya kijambazi likiendelea kushuhudiwa bila wahusika kuchukuliwa hatua.

Ni vyema kukumbuka kuwa mnamo Aprili, dereva wa Dkt. Musumba aliuawa katika mazingira kama hayo, huku mke wa Dkt. Musumba akijeruhiwa vibaya katika tukio hilo.

Dkt. Musumba atakumbukwa kwa kujitolea kwake kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wote wa eneo la Karisimbi. Kifo chake kimeacha majonzi makubwa kwa familia yake, jumuiya ya madaktari na wakazi wa Goma, ambao sasa wanaishi kwa hofu kutokana na ongezeko la uhalifu wa mtaani unaotishia ustawi wa huduma za afya katika mji huo.

Mwandishi: MANGWA