Mshauri wa Trump Atoa Maoni Kuhusu Kurudi kwa Joseph Kabila Katika Siasa za Congo

Katika mahojiano aliyoyafanya hivi karibuni na Jeune Afrique, Massad Boulos, mshauri wa masuala ya Afrika wa rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ametathmini kwa uangalifu kurudi kwa Joseph Kabila kwenye ulingo wa siasa za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alipoulizwa kuhusu kuongezeka kwa harakati za kisiasa za Kabila pamoja na mashauriano anayofanya hivi sasa huko Bukavu, mashariki mwa nchi, Boulos alichagua kutoa majibu ya tahadhari huku akionesha shaka juu ya ushawishi halisi wa rais huyo wa zamani.

“Je, ana ushawishi mkubwa kweli? Ni mmoja wa wadau, lakini hili ni suala la ndani kabisa. Ni watu wa Congo pekee wanaoweza kuamua hilo,” alisema Boulos.

Kauli hii inakuja wakati Joseph Kabila, ambaye alijiondoa katika siasa za moja kwa moja tangu alipomkabidhi madaraka Félix Tshisekedi mwaka 2019, anaendelea na mikutano ya mara kwa mara ya kisiasa katika eneo la Sud-Kivu, ambalo pia linakabiliwa na changamoto ya uasi wa kundi la M23.

Hatua ya Kabila imeibua maswali mengi na uvumi kuhusu mustakabali wake wa kisiasa.

Kutoka upande wa Marekani, matamshi ya Boulos yanaonesha kuwa Washington haina mpango wa kuingilia moja kwa moja mjadala huu wa ndani wa Congo, ingawa inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kisiasa wa taifa hilo, hususan katika muktadha wa mvutano unaoendelea kanda ya Maziwa Makuu.

Mwandishi: MANGWA