
🔴 RDC : Joseph Kabila Aanzisha Mashauriano Bukavu kwa Ajili ya Kutafuta Amani Mashariki mwa Nchi
Bukavu, 25 Juni 2025 – Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (RDC), Joseph Kabila, ameanza rasmi duru mpya ya mashauriano na makundi ya kijamii katika mkoa wa Kivu Kusini, akiwa kwenye ziara yake mjini Bukavu.
Katika siku ya Jumatano, Kabila alikutana na machifu wa kimila kutoka chefferies na makundi mbalimbali ya kijamii katika mkoa huo. Kwa mujibu wa viongozi waliokutana naye, mazungumzo hayo yalijikita kwenye mada kuu ya utafutaji wa amani katika eneo la mashariki ambalo limekuwa katika hali ya machafuko kwa zaidi ya miongo mitatu.
Joseph Kabila amesema lengo kuu la ziara yake ni kusaidia juhudi za kurejesha amani na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Kivu Kusini na mashariki kwa ujumla.
Viongozi wa kimila waliohudhuria mkutano huo walieleza kuwa walitumia nafasi hiyo kumueleza Kabila matarajio ya watu wao kuhusu amani ya kudumu na kumhimiza kuendelea kushiriki katika juhudi za kutatua mgogoro unaoendelea.
Ziara ya Kabila Bukavu inakuja wakati ambapo eneo hilo linaendelea kushuhudia mvutano wa kiusalama, huku juhudi mbalimbali za ndani na kimataifa zikiendelea kufanyika ili kumaliza migogoro ya muda mrefu inayolikumba eneo la mashariki mwa DRC.
Muandishi: MANGWA
#RDC #JosephKabila #Bukavu #KivuKusini #AmaniMashariki
