Screenshot

🔴 MAHAKAMA YA JUU gYA MAREKANI YATOA RUHUSA KWA UTWALA WA TRUMP KUWAFUKUZA WAHAMIAJI KWA NCHI NYINGINE

Mahakama ya Juu ya Marekani imeidhinisha rasmi sera ya utawala wa Rais Donald Trump ya kuwarejesha wahamiaji kwa nguvu katika nchi nyingine tofauti na walikotoka. Uamuzi huo ulitolewa Ijumaa hii kwa kura 6 dhidi ya 3, huku majaji wa mrengo wa kihafidhina wakiunga mkono hatua hiyo na majaji wa mrengo wa kiliberali wakipinga vikali, wakisema kuwa hatua hiyo ni uvunjaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Majaji waunga mkono hatua ya serikali

Katika uamuzi huo, Mahakama ya Juu imebatilisha agizo la awali lililotolewa na Jaji wa Wilaya ya Boston, Brian Murphy, ambalo lilitaka wahamiaji kupewa nafasi ya kueleza sababu zao kwa nini wasihamishwe hadi nchi nyingine wanazoona kuwa hatarishi kwao.

Utawala wa Trump ulikuwa umesema kuwa wahamiaji waliokuwa wameondolewa mwezi Mei – kutoka Myanmar, Sudan Kusini, Cuba, Mexico, Laos, na Vietnam – walikuwa ni “watu hatari sana” na kwamba kuondolewa kwao ni kwa ajili ya usalama wa taifa.

Majaji wa Kiliberali walalamikia ukiukwaji wa haki

Majaji watatu wa upande wa kiliberali walipinga uamuzi huo wakisema kuwa serikali haiwezi kuwahamisha wahamiaji kwa nguvu kwenda nchi yoyote bila kuwapa fursa ya kueleza hatari wanazoweza kukutana nazo. Walisema kuwa huu ni uvunjaji wa haki za msingi za binadamu na ni “kuhalalisha uvunjaji wa sheria.”

Jaji Murphy aliamua mwezi Aprili kuwa hata kama wahamiaji hao walishindwa rufaa zao katika mahakama zingine, walipaswa kupewa haki ya kujieleza kuwa wanaweza kuteswa au hata kuuawa katika nchi wanakopelekwa. Hata hivyo, Mahakama ya Juu sasa imefuta uamuzi huo na kuruhusu serikali ya Marekani kuwaondoa mara moja.

Sera ya uhamiaji ya Trump yazidi kuchukua kasi

Hii ni sehemu ya msimamo mkali wa utawala wa Donald Trump katika kupambana na wahamiaji, ambapo mara kadhaa amesisitiza kuwa wahamiaji haramu ni tishio kwa usalama wa Marekani. Uamuzi huu wa Mahakama ya Juu unampa Trump ushindi mkubwa katika ajenda yake ya kudhibiti uhamiaji.

Wataalamu wa sheria za kimataifa na mashirika ya haki za binadamu wameeleza wasiwasi wao kuwa uamuzi huu unaweza kufungua mlango kwa ukiukwaji zaidi wa haki za wahamiaji, na kuweka maisha ya maelfu ya watu hatarini.

Kwa sasa, bado haijajulikana ni nchi zipi nyingine zinalengwa kwa ajili ya kuwahamisha wahamiaji hao, lakini vyanzo vya ndani vimeeleza kuwa ndege ya kwanza iliwasafirisha baadhi yao kwenda Sudan Kusini – nchi inayokumbwa na migogoro na ukosefu wa usalama wa muda mrefu.

Tunaendelea kufuatilia kwa karibu.

Muandishi: MANGWA