🔴 Jeshi la Rwanda Lakanusha Taarifa za Uongo Kuhusu Afya ya Rais Paul Kagame

Jeshi la Rwanda limetangaza rasmi kwamba taarifa zinazodai kuwa afya ya Rais Paul Kagame iko katika hali “hatarini sana” ni za uongo na zisizo na msingi. Kauli hiyo imekuja kufuatia wimbi la uvumi lililoenea kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari, kuhusu hali ya kiafya ya Rais Kagame, ambaye hakuonekana hadharani kwa karibu wiki tatu mfululizo.

Taarifa hizo zilianza kusambaa baada ya David Himbara, mpinzani anayeishi uhamishoni na ambaye alikuwa mshauri wa masuala ya kiuchumi wa Kagame, kudai kuwa Rais Kagame ni mgonjwa na yuko nchini Ujerumani kwa matibabu. Himbara alieleza kuwa kutokuwepo kwa Kagame katika shughuli za hadhara ni ishara kuwa kuna jambo kubwa linalofichwa.

Hata hivyo, Serikali ya Rwanda kupitia msemaji wake Yolande Makolo, imekanusha vikali madai hayo, ikisema kuwa Rais Kagame yuko salama na anapumzika kama binadamu yeyote anayehitaji muda wa kupumzika. Gazeti la Rwanda la Taarifa lilimnukuu Makolo akisema:

“Rais yuko vizuri na anapumzika kawaida. Ni binadamu kama sisi sote na ni jambo la kawaida kwa mtu kuchukua muda wa kupumzika baada ya kazi nyingi za kitaifa.”

Makolo aliongeza kuwa wananchi wa Rwanda hawapaswi kuyumbishwa na taarifa za uongo ambazo zinakusudia kuleta taharuki na sintofahamu miongoni mwao. Kwa upande wake, jeshi la Rwanda limeweka wazi kuwa taarifa hizi ni uzushi ulioenezwa kwa makusudi, na kwamba hakuna changamoto yoyote kuhusu afya ya Rais wao.

Rais Paul Kagame alionekana hadharani kwa mara ya mwisho tarehe 6 Juni 2025 alipokutana na wanafunzi wa Hope Haven Christian School mjini Kigali, katika shughuli ya kijamii iliyopeperushwa na vyombo vya habari vya serikali. Tangu siku hiyo, hakuonekana tena kwenye matukio ya umma, jambo ambalo liliibua maswali miongoni mwa wananchi na wafuasi wa upinzani.

Licha ya juhudi za BBC kuwasiliana na ofisi ya Rais ili kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu hali hiyo, hadi sasa ofisi hiyo haijatoa majibu rasmi.

Kwa sasa, serikali ya Rwanda imewaomba wananchi na jamii ya kimataifa kutotilia maanani taarifa zinazozagaa bila uthibitisho rasmi.

Muandishi: MANGWA