Tehran, Juni 2025 – Katika kile kinachoonekana kama kuporomoka kwa mkakati wa muda mrefu wa Iran kuimarisha ushawishi wake kupitia vikundi vya wapiganaji Mashariki ya Kati, makundi yaliyokuwa sehemu ya kile kilichojulikana kama “Axis of Resistance” yameanza kujiondoa na kutoshiriki kikamilifu katika mzozo wa kijeshi dhidi ya Israel.

Kwa miongo kadhaa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikiwekeza katika kujenga mitandao ya wanamgambo yenye nguvu katika Gaza (Hamas), Lebanon (Hezbollah), Yemen (Houthi), Iraq, na Syria. Lengo lilikuwa kuizunguka Israel kwa maadui kutoka pande zote, lakini hali imebadilika ghafla.

Kulingana na ripoti ya Wall Street Journal, makundi haya kwa sasa yanaangalia zaidi usalama wao kuliko kushiriki moja kwa moja katika mzozo. “Kwa mitandao hii yote ya wapiganaji, sasa si wakati wa mapambano. Ni wakati wa kuweka kichwa chini na kusalimika,” anasema Renad Mansour, mtaalam mwandamizi kutoka taasisi ya Chatham House.

Mashambulizi dhidi ya Hamas yamevuruga mizani

Hamas, ambayo ndiyo ilikuwa kiungo kikuu cha Iran katika Gaza, imepigwa vikali na majeshi ya Israel tangu vita kuanza. Zaidi ya wapiganaji 20,000 wameuawa, na miundombinu ya kijeshi ya kundi hilo imeharibiwa kwa kiwango kikubwa. Hili limewavunja moyo washirika wengine wa Iran.

“Wengi wamepoteza imani kuwa Iran inaweza kuwasaidia kama inavyodai. Wameona jinsi Hamas ilivyopigwa, na sasa hawataki kuwa mfuata nyuki waangamie naye,” anaongeza Mansour.

Houthi na Hezbollah wakwama

Wakati Houthi kutoka Yemen wanaendelea kudai kuwa wanaunga mkono Iran, mashambulizi yao yamekuwa ya kawaida na hayajaleta tishio la kweli. Nao Hezbollah wa Lebanon wameripotiwa kuwa na wasiwasi mkubwa wa kushambuliwa vikali na Israel, hivyo hawajachukua hatua kali kama ilivyotarajiwa.

Iran yabaki peke yake

Hali hii inaashiria upweke mkubwa kwa Iran, ambayo ilikuwa inajivunia kuwa na ushawishi mkubwa wa kijeshi katika eneo. Sasa, Iran imebakia bila washirika wa kweli katika vita vinavyozidi kuongezeka dhidi ya Israel, na dunia inaangalia kwa wasiwasi kama hili ni mwisho wa hadithi ya “Axis of Resistance.”

Huku vita vikizidi kushika kasi, wachambuzi wa kimataifa wanaamini kuwa hali hii ni kengele ya tahadhari kwa Tehran, ambayo sasa italazimika kufikiria upya mkakati wake wa kisiasa na kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

✍🏽 Mwandishi: MANGWA

#MasharikiYaKati #Iran #Israel #Hamas #Hezbollah #Houthis #AxisOfResistance #HabariLeo #MecaMedia #MANGWA