
Malabo, 6 Juni 2025 – Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Félix-Antoine Tshisekedi, amehudhuria kwa mara nyingine kikao cha 26 cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (CEEAC), kilichofanyika katika jiji la Sipopo, kisiwa cha Bioko, nchini Guinea ya Ikweta.
Kikao hicho kiliongozwa kwa kauli mbiu: “Kudumisha mafanikio ya mageuzi ya CEEAC ili kuharakisha ujumuishaji wa kikanda na ujenzi wa jamii yenye hatma ya pamoja Afrika ya Kati.”
Miongoni mwa ajenda kuu zilizojadiliwa ni:
Hali ya usalama mashariki mwa DRC, Mchakato wa kubadilishana uongozi wa muda wa CEEAC, Hatima ya kikosi cha uongozi wa Tume ya CEEAC.
Baada ya hotuba za viongozi wa taasisi mbalimbali kama UN, Umoja wa Afrika, Tume ya CEEAC na mwenyeji Rais Obiang Nguema Mbasogo, mkutano uliendelea kwa kikao cha faragha kilichodumu kwa zaidi ya saa tatu.

Maamuzi Muhimu ya Mkutano:
Kwa suala la mashariki mwa DRC: Viongozi wa CEEAC walitambua rasmi uvamizi unaofanywa na Rwanda dhidi ya DRC na wakatoa agizo kwa Rwanda kuondoa mara moja majeshi yake katika ardhi ya Kongo. Uongozi wa CEEAC: Ili kuepuka mgongano wa kimaslahi, Guinea ya Ikweta itaendelea kushikilia uenyekiti wa muda wa jumuiya hiyo badala ya Rwanda hadi mgogoro wake na DRC utakapopatiwa suluhu. Uongozi wa Tume ya CEEAC: Ilikubaliwa kuwa viongozi wa sasa wa tume hiyo wataondoka baada ya miezi mitatu, ambapo mchakato wa kuteua uongozi mpya utaanza.
Rais Tshisekedi aliandamana na ujumbe wa juu wa serikali, akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda Didier Manzenga, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Grâce Yamba, Mwakilishi Mkuu wa Rais Sumbu Sita, na Balozi wa DRC nchini Guinea ya Ikweta Jocelyne Kabengele.

